

TV ya INJILI Kwenye Internet
-
WWW.GOSPELGTV.COM
Tel.
254722602445 E-mail:
munishi@munishi.com or info@munishi.com

TELKOMKenya
Wazinduka usingizini

Walizoea ukiritimba wa kuwa peke yao, ndiyo maana kupata simu enzi
zao ungebidi uwaonyeshe vitu vingi sana.Kuanzia kitambulisho, cheti
cha kuzaliwa na PIN namba. Tena ungejaza fomu inayokutaka useme kama
una kazi au la. Na kama unayo, useme ni kazi gani na kwa nini ufanye
kazi hiyo.Ukifikiri vikwazo vya kupata simu vitaishia hapo, wanakuambia
uwaletee picha tatu saizi ya paspoti, na tena ziwekwe saini ya wakili
wa serikali nyuma kuthibitisha kama kweli ni wewe. Hata kama una alama
nyingi usoni kama mimi, bado wangesisitiza uwaletee picha tatu. Na
hiyo ni fomu ya ombi la kuwekewa simu nyumbani au ofisini.Iliwabidi
wengi wayapitie mateso yote hayo ili tu siku moja wajikute wanaweza
kuwasiliana kutumia kifaa kiitwacho simu, au TELLEPHONE kama wanavyoziita
wale waliotutawala miaka arobaini iliyopita. Waliokuwa na uwezo walikwepa
vizingiti vyote hivyo kwa kuwauliza wafanyikazi wa Posta wawaambie
ni pesa ngapi wangetaka ili mtu apate simu bila kuruka virunzi vyote
hivyo. Hapo RUSHWA ikaota mizizi katika shirika hilo kwa kiwango cha
kutisha. Wengi wakati huo walikata tamaa na hawakujaribu kukanyaga
ofisi za TELKOM wakati huo walkiitwa Kenya Posta.


Nani Zaidi?

Kama wasemavyo waswahili "Kilicho na mwanzo hakikosi mwisho wake,
Hakuna mtu aliyetarajia kwamba maringo na makidai ya shirika la Posta
yangefikia kikomo siku moja. Hao hao waswahili wana msemo kwamba "Upole
wa paka usikudanganye umpige bila kumwachia mwanya wa kutorokea. Ukifanya
hivyo, macho yako yatakuwa ndiyo mwanya.Ataruka kima usawa na macho
yako, na kingine utakachokiona ni giza totoro baada ya macho yako
kukumbana na kucha kali za paka." TELKOM hawakuomba iwe hivyo
kwao, Lakini sijui SAFARIOM na CELTEL walitokea wapi, wakafanya kile
ambacho paka angefanya. Waliruka kima usawa wa macho ya TELKOM, Wakawamwagia
vumbi zito, kiasi kwamba hawakuyaamini macho yao kibiashara kwamba
yamezimwa. Walijikuta pale ambapo wananchi walikuwa kila siku wanapozuru
ofisi za TELKOM. Kuomba kwa magoti uwekewe simu, ikawa sasa ni zamu
yao kuwaomba wateja kwa magoti wakubali kuwekewa simu.

Hata hivyo
walisahau kwamba aliyekwisha umwa na nyoka, huogopa kusogelea hata
kijiti kinachofanana na nyoka. Nilijikuta nikiogopa hivyo mjini Nairobi
hivi majuzi wakati nilipowakuta TELKOM wakiwa wameweka kibanda nje
na wanawabembeleza wateja wakubali kuunganishwa katika simu zao ambazo
sasa ni bila waya. Yaani ni ile ile simu iliyokuwa inawekwa kwako
kutumia waya mrefu kutoka mbali, sasa unaipata kwa kununua kadi simu
mfano wa zile za simu za mikononi. Na pia kifaa utakachoweka smu kadi
hiyo, kinafanana kabisa na kile wanachotumia wakali wao kina SAFARICOM
na CELTEL. Tofauti ni masafa. Usijali kama ulikuwa unajua kwamba simu
za mikononi tunazotumia hupeperusha mawasiliano zikitumia masafa ya
GSM. La muhimu kwa wengi ni simu iongee, na wao wawasiliane.Hayo ya
GSM na CDMA hayawahusu wengi. Wala hawapotezi muda kutaka kujua. Hata
mimi ni vivyo hivyo, lakini nilijikuta nikikaa chini nipewe somo na
wana TELKOM.

Kwanza walinikaribisha
vizuri sana katika kibanda chao. Hiyo ikanitia mashaka kwa sababu
ninawajua tangu enzi zao za KENYA POSTA.. "Karibu sana tuna tekniloji
mpya hapa ambayo inakuwezesha kuwa na Land Line MObile." Nilijivuta
ndani sawa sawa niweze kusikia jipya." Unaona kwamba sisi TELKOM
tumeamua kuwakomboa kutoka utumwa wa SAFARIKOM na CELTEL. Ukiwa na
shilingi elfu moja tunakuuzia simu kadi. Ukitaka kuunganishwa lazima
ununue simu ya mkononi lakini inayotumia masafa ya CDMA." Alisema
dada mmoja mama wa makamo kidogo, jambo lililoashiria kwamba amekuwepo
tangu enzi zile.Niliduwaa kidogo baada ya kutajiwa CDMA, lakini nikajikaza
kisabuni na kuuliza nifahamishwe zaidi.Waswahili husema kuuliza siyo
ujinga. Ndipo nilipopewa somo kwamba CDMA ni teknoloji ambayo imekuwepo
zaidi ya miaka mia, na imekuwa ikitumika na majeshi hasa ya Amerika.Sasa
huendaikawa majeshi hayo yamepata teknolojia mpya ndiyo maana wameamua
kuacha CDMA itumike kwa mawasiliano ya kibiashara. Nikakumbuka stori
kama hiyo nilipokuwa nikinunua simu yangu ya mkononi ya kwanza.Tofauti
ya ile ya kwanza ni GSM.

Sasa kabla sijakuchanganya
na hizi lugha za tekniko, hebu nikuambie nilivyoambiwa yaishe. Waliniambia
kwamba ninaweza kununua simu ya CDMA kwa Kshs. 7,000 na nitaweza kuitumia
simu yangu kama vile ningetumia simu ya kawaida ya LAND LINE. Bei
ni chini ukilinganisha na SAFARICOM na wenzao KENCEL. Tena walisema
ukiwa na simu hiyo ya CDMA itakuwezesha kuingia kwenye mtandao wa
kompyuta duniani yaani INTERNET kwa bei ile ile ya kupiga simu 'LOKOL.'
Nilijikuta ninashawishika, kwani mimi mara nyingi hupenda kuingia
kwenye mtandao kuandika story kama hii unayoisoma. Mara nyingi huandika
usiku baada ya kazi nyingine za mchana, na ingekuwa vizuri kwangu
kama ningeweza kuingia kwenye mtandao wakati wowote na kwa bei nafuu.
Kwa hilo tu kwamba nitaingia kwenye INTERNET na nitalipa dakika za
simu pekee bila kulipia Internet, tena kwa bei ya 'LOKOL', niliona
kwamba TELKOM wako sawa kibei kuliko makampuni mengine.Tena wanadai
kwamba ukijiunga kwenye mtandao kutumia sava zao, utapata kile unachokitaka
kwenye Internet upesi kwani tovuti yao ina mbio kali.Hilo sikumeza
kabisa hapo kwa hapo, bali niliwaambia nikiweza kuingia kwenye mtandao
na nione kweli mbio wanayoisema iko, hapo nitawaamini. Nilinunua simu
kadi yao Kshs.1,000 huku nikilalamika kwamba kama kweli wamekuja kututoa
utumwani, basi hata bei ya simu kadi bado iko juu. Nilipotaka waniuzie
pamoja na simu, walinielekeza kwa wauzaji wa simu. Hapo niliona ujanja
wa TELKOM. Hawataki kuhusika na uuzaji wa simu ndiyo maana wamewapa
tenda kampuni binafsi kufanya kazi hiyo.
Hapa ni mtambo wa CDMA ambao TELKOM wanasema utayabadili maisha
ya Wakenya. Kutumia simu hii kutamuwezesha mteja kupiga simu kwa bei
ya land line japo ni Mobile. Tena kuunganishwa kwenye mitambo ya INTERNET
haijawahi kuwa rahisi hivi. Ukiwa CDMA kompyuta yako inaunganishwa
na zile nyingine ulimwenguni kote kutumia mtandao wa INTERNET.
Nikanunua simu
ya CDMA Nokia 6602 kwa bei ya Kshs.7,100 Bado hata hapo nililalamika
kwani simu ya kiwango hicho lakini ni GSM bei yake ni ndogo mara mbili
ya hiyo ya CDMA. Hilo pia niliwaambia. Nikawalipa pesa. Nikapewa risiti
ya simu. Kabla nipewe risiti ya simu kadi, wakaleta fomu ya kujaza.
Nilipoitupia macho nikakuta ina karibia zile za enzi zile japo hii
haitaki picha tatu. Lakini kuna sehemu inayokutaka ujaze ulizaliwa
lini. Hapo niliona nisikae kimya. Niliwauliza hii wanayoiita teknoloji
mpya inawabagua watu waliokula chumvi nyingi kama mimi? Na ni kwa
nini watake kujua miaka yangu? CDMA na umri wa mtu vinaingiliana wapi?
Nikajua bado yale ya enzi zile hayajawatoka kabisa. Nikajipa moyo
na nikajaza miaka yangu na wakanipa simu kadi. Nilipoiweka kwenye
CDMA yangu na kuona kwamba ninaweza kuwasiliana na mtu kwa land line
Mobile yangu, nilifurahi utadhani nilipewa zawadi. Lakini ukilinganisha
na mateso ambayo mtu alipaswa kuyapitia ndipo apate simu enzi zile,
siyo ajabu ukimuona Munishi akicheka mpaka jino la mwisho kuonekana.
Ni ajabu kwake kuona wabembelezwa wakibembeleza.Tena ni ajabu kuona
kwamba simu ambayo ungeweza kuomba na ikachukua mwaka na wakati mwingine
hata miaka miwili bila kupata, sasa unanunua na unakwenda ukiongea.
Furaha yangu haikudumu sana kwani kufika nyumbani simu yangu ya CDMA
ikaleta kasheshe. Nikipiga, niliyemwita namsikia lakini yeye hanisikii.
Nilipowaita watu watatu na tatizo likawa ni hilo, nilijua nimeliwa.Kuangalia
risiti nikakuta nambari ya simu ya wenye kampuni ya uuzaji wa CDMA.
Nilipojitambulisha, na hapo nilikuwa natumia GSM ya SAFARICOM, Nikawaeleza
tatizo langu na CDMA. Wakawa watu wazuri sana. Walinitaka nirudi pale
pale niliponunua simu ili waikague na kisha wanipe nyingine. Kweli
kesho yake nilipofika waliikagua simu na wakanipa nyingine bila kulipa
chochote. Nilipowauliza jinsi ya kuiunganisha CDMA na kompyuta yangu
ili niweze kuingia kwenye mtandao wa INTERNET waliniambia inatakiwa
kebo maalum ambayo hawana.Tena kutaitajika 'SOFT WEAR' ambayo hawana.
Tena kutahitajika kuinstol hiyo soft wear pamoja na kukomfiga, ambayo
pia hawajui kuifanya.

Hapo ndipo
niliposema Mungu nisaidie. Ikiwa wenye CDMA hawajui inafanywaje, mimi
nitafanikiwa kweli? Nilikumbuka msemo ule ule. "Aulizaye siyo
mjinga." Nilianza kuwauliza marafiki wenye ujuzi na kompyuta
kuliko mimi, na mmoja wao akaniambia hiyo ni rahisi sana. Alijigamba
kwamba makampuni yote yanayojihusisha na CDMA bado jinsi ya kuunganisha
simu ndogo za CDMA na kompyuta inawapiga chenga. Na kwa sababu wao
siyo kama Munishi, wanaogopa kuuliza. Na hata wakijua unajua, hawataki
kujiaibisha waonekane kampuni kubwa kama hiyo inaingizwa mjini na
kitu kidogo kama "DRIVER za kuifanya simu ya CDMA iwe 'MODERM."
Baada ya kusema hayo, nawapongeza TELKOM kwa kuzinduka usingizini.
Lakini itawabidi wawe makini kwani kibarua kilicho mbele yao ni kigumu.
SAFARICOM na CELTEL wamekita mizizi kiasi kwamba wakisikia TELKOM
wameamka, hawatasita kuteremsha bei na kuifanya huduma ya INTERNET
kuwa rahisi kupitia masafa ya GSM. Naomba Mungu anipe uhai ili nione
na hayo pia.

Tofauti na Enzi zile za kuletewa bili za uongo, sasa unanunua kadi
ya kiwango unachopenda. Ukitumia salio liishe, huwezi kuwasiliana
tena.Ila bado kuna wasiwasi kama watakuwa waaminifu walipishe kama
wanavyosema na siyo kama wapendavyo.Ukiweka pesa kwenye akaunti yako,
sijui utajuaje umetumia kiasi gani kwani TELKOM bado hawatumi ujumbe
mfupi kuonyesha salio.Badala yake ujumbe wa sauti inayokoseakosea
hukwambia salio lako.Wengi wanasema ingekuwa bora wawe na uwazi. Hasa
mtu anapojiunga kwenye internet ni vigumu kujua ni wakati gani wanapoanza
kukulipisha. Je ni wakati tayari ukurasa wa Internet umefunguka? au
hata wakati wa kujaribu kuunganishwa unalipishwa? Niliweka mia nne
na ziliisha kabla sijafanikiwa kuingia kwenye internet. Sikujua ziliishia
wapi. Hapo napo kuna kibarua upande wa TELKOM ili warudishe imani
kwa wateja. Huku hayo yakijiri, Bado kuna makampuni mawili yanayoshindana
na TELKOM katika masafa ya CDMA. Kampuni kama FLASHCOM na POPOTE wanawapa
TELKOM kichefuchefu na kukosa usingizi. Lakini kwetu wateja ni furaha.
Kwani wanaposhindana, bei zitakuja chini na itakuwa rahisi kuwasiliana.

Hawa ni FLASHKOM. Pia wao hutumia CDMA. Ila kimasafa wanatofautiana
na TELKOM ndiyo maana hata simu zao zinatofautiana. Lakini tuwape
muda.Sitoshangaa kuona sokoni simu moja inayotumia masafa yote. Yaani
GSM na CDMA zote pamoja kwenye simu moja.Tayari ukienda River Road
kuna wataalam wanaoweza kuifanya simu yako ya GSM iweze kufanya kazi
kama CDMA. Tatizo bado ni bei zao. Ukiwasikiliza utakuta kuna ujanja
ujanja ndani. Watakwambia ni Internet inaanzia Kshs.2000 kwa mwezi.
Ukisisimka useme haya chukueni elfu mbili wanakuambia ngoja kwanza.
Hiyo haitoshi. Lazima ulipe deposit ya kiwango kama hicho. Tumbo linaanza
kuingia baridi. Na kwa sababu anayekueleza hivyo ni msichana mrembo
aliyesomea kazi ya kuuza kila kitu, unaona usimkosee kiumbe kama huyo.
Unasema haya basi nimeongeza elfu mbili ziwe nne. Unauliza huku sauti
ikianza kukwaruzana kwani haukuwa tayari kutumia kiwango hicho cha
pesa. Je nikilipa hiyo nitapata huduma ya Internet kwa mwezi mzima?
Unaambiwa ndiyo lakini..... Jasho jembamba linaanza kukutoka ukitaka
kusikia lakini ni ya nini tena Yarabi? Wanakuambia ukilipa hizo pesa
utaweza kuingia kwenye mtandao masaa ya usiku pekee. Mchana wote ukitaka
kuingia kwenye Internet, ni lazima ulipie masaa mchana. Unaanza kusikia
kizunguzungu. Unauliza. Nitalipaje? Unaambiwa utaletewa bill baada
ya kujaza fomu na kusaini mkataba na FLASHCOM. Machoni kweli unaona
vitu kama vinaflashflash. Kama akili yako inafanya kazi haraka kama
ya sungura, unasema sitaki. Rudisheni pesa zangu. Mbona kuna ujanja
ujanja mwingi? Si muifanye rahisi tu? Mbona isiwe bei moja kwa wote?
Yaani wale wanaotaka kununua kadi za kukwaruza wanunue za kiwango
wanachoweza, Na wale wasiotaka usumbufu wanunue kiwango cha mwezi
mzima? Hapo unatakiwa uwazi tu. Kwamba Internet kwa mwezi ni shilingi
kadhaa. Lakini sharti liwe ni kulipa hizo pesa kabla hujaanza kutumia.
Hiyo itaokoa mambo mengi ya kutuma na kupokea bill ambazo lazima kuwe
na watu wa kuthibitisha ni za kweli. Japo hata kununua jumla kuna
hatari zake, lakini siku hizi kuna programu zinazoweza kuonyesha mtumiaji
wa simu aliitumia vipi.Hiyo ingetufanya sisi kina yahe, tusiotaka
kutumia pesa zote kwa simu kujipanga. Lakini kwa mtindo huu wa ujanja
ujanja mwingi wa wale waliosomea kuuza, wengi bado tutakimbilia kwenye
vibanda vya Internet ambayo vinatoza senti hamsini za Kenya kwa dakika
moja. Yaani ukiwa na senti hamsini unaweza kuingia kwenye mtandao
Kenya. Hii ni tofauti kabisa na vibanda kama hivyo nchini Tanzania.
Huko wanakulazimisha kukaa nusu saa hata kama shughuli yako itakuwa
imemalizika baada ya dakika tano. Wanakupa kibarua kigumu cha kuamua
kusuka au kunyoa. Yaani ukimaliza kabla ya nusu saa uwalipe nusu saa
na uende.Au ukae hapo ukiiangalia kompyuta yao kama huna la ziada.Isitoshe
makampuni ya simu Tanzania yanalipisha kwa dola na siyo shilingi za
Tanzania. Kisa wanasema shilingi ya Tanzania imeshuka thamani mpaka
kompyuta za makampuni ya simu zinakataa kuwalipisha watu kutumia shilingi.
Hebu nirudi Kenya kwa FASHCOM. Ukishanunua kadi za kukwaruza na uweke
kwenye simu yako bado kuna kibarua cha kuwatafuta wajanja wa River
Road wakuuzie kebo itakayoiunganisha simu yako na kompyuta yako ili
uweze kuingia kwenye mtandao. Usiniulize kwa nini Kampuni inayojigamba
kuwa ya kwanza kuleta CDMA Kenya haina wataalam pamoja na kebo za
kuwaunganisha wateja. Hiyo inashangaza kwani wengi tungetegemea kupata
usaidizi wote kuhusu CDMA hapo FLASHCOM. Kwamba ni lazima uupate kwingineko
hiyo inafanya mambo kuwa magumu. Mfano ni wakati umetafuta kila kitu
na hatimaye kompyuta yako ikaweza kuonana na simu kisha kujiunga kwenye
mtandao. Hapo unatakiwa uombe Mungu chochote kisiende mrama. Endapo
mawasiliano na mtandao yatakatika ghafla utashindwa nani wa kuuliza.
Yule wa River Road, au Wanaojiita mainjinia wa Flashcom? Yaliponikuta
hayo, niliamua kwanza nimuulize mtaalamu wangu. Kwamba aliweza kuifanya
simu yangu ionane na kompyuta yangu kisha nikaweza kuunganishwa kwenye
mtandao kupitia FLASHKOM, kwangu huyo ndiye mtaalam wa kweli. Nilimuuliza
vipi naingia kwenye mtandao na sioni ukurasa ukifunguka? aliniuliza
ninapata ujumbe gani kwenye ukurasa uliokataa. Nikamwambia inasema
ukurasa hauwezifunguka. Mara moja akajua tatizo ni Flashcom ndio hawako
kwenye mtandao wakati huo. Sababu inaweza kuwa watoa mtandao wamekatiwa
mtandao kwa kukosa kuwalipa wanaowapa huduma hiyo, au iwe ni hitilafu
za mitambo. Nilipojaribu kuwapigia FLASHCOM nijue kulikoni, wao walijaribu
kuuzunguka mbuyu badala ya kusema kweli hawako kwenye mtandao. Watakwambia
nenda kwenye internet OpKwa FLASHCOM ni mwanzo mzuri na tunawatakia
kila la kheri.
Huu ndio mtambo wa CDMA wanaotumia kampuni ya FLASHKOM. Tofauti
na ule wa TELKOM, huu kidogo bei yake iko chini. Ukiwa na Kshs. 4500
unaweza kupata simu ya CDMA inayoweza kufanya na mitambo ya FLASHCOM.
Ila sim card za Flashcom ni Kshs.1,500. Ila kuna tatizo linalowakumba
wote. Network zao bado ziko Nairobi pekee. Ukitoka nje ya Nairobi
kidogo tuseme uwe Ngong, Network inaanza kupotea. Mwenyewe nilinunua
Land line Mobile ili niweze kuingia kwenye internet usiku baada ya
kazi, lakini kwa mshangao nimekuta kwamba sehemu ninayoishi ya Ngong
bado masafa yao ya CDMA hayafiki sawasawa. Bado wanahitajika kuvuta
soksi zao ili waweze kutangaza kwamba wamekuja kututoa kwenye utumwa
wa SAFARICOM na CELTEL. Vinginevyo Safaricom wakipunguza bei kidogo,
na wawaruhusu watu kuingia kwenye mtandao kwa bei nafuu, wengi watachagua
kubakia utumwani, kwani waliuzwa huko na hao hao wanaojaribu kuwatoa
huko.
Nao Safaricom ni kama wanachunguza kila hatua wanayochukua kina TELKOM
na FLASHCOM ili waje na sunami ya bei itakayowafanya wapinzani waone
vumbi mbele yao. Tunasubiri tuone Wakenya wakielekea mahali pa kupiga
simu bure kama siyo kutuma jumbe fupi bure, au zote pamoja.

Celtel wamekazana kuunganisha mtandao
Afrika ya mashariki. Wanachosahau ni kwamba watumiaji wa simu za mikononi
Uganda na Tanzania pamoja hawafikii idadi ya watumiaji simu hizo Kenya.
Sababu kubwa ikiwa bei za simu Uganda na Tanzania ni ghali ikilinganishwa
na Kenya. Tanzania kuongezea salio lako ni lazima ufanye hivyo kwa
dola na siyo shilingi za Tanzania. Inasemekana makampuni ya simu yalidaiwa
rushwa ya kiwango cha juu na watawala Tanzania, na mzigo huo wanawabebesha
watanzania. Usijali kwamba Tanzania na Uganda ndio walioanza kuwa
na simu za mkononi, lakini msemo "Kutangulia siyo kufika"
utamaanisha sana hasa kwa Tanzania.
Badala Celtel watumie mabilioni kuunganisha
mtandao, wangepunguza bei zao ziwe chini ya zile za Safaricom na watu
wote wangehamia huko na na kupiga simu Afrika ya mashariki ingekuwa
rahisi. Endapo bei Celtel zitabaki kama zilivyo, basi wapinzani wao
wa jadi Safaricom wataendelea kutamba sana Kenya ambako soko la simu
ni kubwa kuliko masoko mawili ya Uganda na Tanzania. Haiingii akilini
kwamba Celtel wanaacha soko kubwa kuliendea soko dogo tena kwa kutumia
mabilioni. Kwa nini mabilioni hayo yasingetumika kuwafanya wateja
wa Celtel kupiga simu bure kwa miezi miwili ili kuvuta wateja zaidi?
Ukweli wa mambo ni kwamba Celtel bei
zao ni juu ukilinganisha na Safaricom. Tena wasisahau kwamba Flashcom
wako uwanjani na bei zao ni chini kuliko wote. Kama wangekuwa na mtandao
unaopita Nairobi, mambo yao yangekuwa mazuri zaidi. Lakini hata soko
la Nairobi pekee linaweza kuwafanya Flashcom waanze kugonga chati.
Tunaomba Mungu amguse Kibaki ili kabla hajamaliza muda wake aunde
serikali ya Uganda Made in Kenya, Halafu ifuatie serikali ya Tanzania
Made in Kenya, halafu roho ya Afrika ya mashariki itakuwa imeshika
joto linalostahili.
Msisahau kwamba yote hayo Kibaki anayaweza
kwani aliunda serikali ya Somalia Made in Kenya na inafanya kazi mpaka
sasa. Hata Sudan aliwaundia Serikali. Msishangae kumuona Munishi siku
moja akiingia kwenye Benzi na serikali yake wakielekea Tanzania kupitia
Namanga. Wakati huo makampuni ya simu Tanzania yatapunguza bei zao
ziwe karibu na bure kwani serikali ya Munishi haitakuwa ikichukua
Rushwa toka kwa makampuni hayo kama serikali ya Kikwete inavyofanya.
Kumbe wanasiasa ndio wanaofanya bei za simu kuwa ghali?



