![]() ![]() |
||
|
Gharama ya kuwa na gari Nairobi Baada ya kisa cha Artur Margaryan, Serikali imeonyesha kuviimarisha vyombo vyake vya usalama ili vionekane kwamba vinafanya kazi ipasavyo. Lakini rushwa bado ni kikwazo kikubwa. Pesa zinazungumza sauti kubwa kuliko Haki. Huwezi kujua mizizi ya rushwa imeota kiasi gani, hadi ukutane na ule unaoitwa mkono wa sheria. Hapo ndipo utakapokutana na watu walio tayari kukudhalilisha kwa kiwango chochote mpaka useme mwenyewe ni bei gani nitoke hapa? Watakusukuma kushoto kulia, watakutusi na mwisho watarudia rudia kukufahamisha kwamba kesi yako faini yake ni kiasi kadhaa, au ufungwe miezi kadhaa, na mwisho watakuambia ukitoa rushwa kiasi fulani utatolewa. Ningesimuliwa haya ningekataa, lakini yalinikuta mwenyewe. Ilikuwa tarehe 20 mwezi wa sita mwaka 2006. Nilikuwa nimetokea Mombasa na nikashika Ngong Road kuelekea Ngong. Kabla nifike makao makuu ya usalama barabarani, kuna barabara ya 'ONE WAY' Lakini magari yanapita mawili. Ya mkono wa kulia inaishia mahali bila taarifa, na ni lazima uifuate kurudi ulikotoka au uombe nafasi ya kurudi kwenye 'LANE' ya kushoto uendelee na safari ya kwenda Ngong. Nikiwa katika kuomba nafasi ya kurudi kushoto, alitokea mwana usalama barabarani aliyekuwa amejificha mbele kidogo akingojea windo la siku hiyo. Aliniamuru nifungue mlango aingine ndani
ya gari langu, na tuliandamana hadi makao makuu ya usalama barabarani
ambako walizuia gari pamoja na mimi. Nilipotaka kujua kosa langu,
waliniambia ni kuyapita magari mengine kihatari. Nywele zilinisimama
nikijua kwamba sikuwa nikifanya hivyo. Kila nilipojaribu kujieleza,
ndivyo nilivyozidi kusukumwa niingie ndani ya 'sell'. Hakuna aliyenisikiliza
hata wale niliodhani kwamba wananifahamu. Nikakumbuka msemo kwamba
usiwahi kuwa rafiki wa askari polisi. Ikibidi hata mke na watoto wake
anaweza kuwakamata ili aongezewe cheo. Ilikuwa saa tatu asubuhi, na
tuliwekwa hapo mpaka saa nane tulipopelekwa mahakamani. Pamoja nami
kulikuwepo madereva wa MATATU pamoja na makondakta wao, bila kusahau
mzee mmoja wa asili ya kiasia ambaye maaskari walikuwa wakimwita 'mhindi'
Kwao ilikuwa ni kama sherehe kuwa na mhindi anayepelekwa mahakamani
kna kwamba haikuwa kawaida yao. Hata ofisa msimamizi wa kituo ambaye
ni Mkikuyu alisikika mara kwa mara akiuliza kama bado yule mhindi
yuko katika msafara wa watu wanaopelekwa mahakamani.Tangu Kibaki ashike
madaraka wakikuyu wamewekwa sehemu muhimu hasa polisi na mahakamani.
Nasikia ni kila mahali, lakini mimi nimeshuhudia hilo Polisi na mahakamani.
Tulipofikishwa mahakamani ndipo tulipoanza kusikia kila mtu akitajiwa kosa lake na faini yake, na kiwango anachopaswa kulipa kama rushwa ili ajinunulie uhuru. Kosa langu niliambiwa adhabu yake ni faini ya shilingi 6000 pesa za Kenya, au nitoe elfu mbili na mia tano niachiwe bila kufikishwa mahakamani. Niliamua liwalo naliwe. Sitatoa rushwa. Baada ya wenzetu kukubali kununua uhuru wao, waliitwa na hatukuwaona tena. Tuliingizwa kwenye seli ya kungojea kwenda mahakamani, na hapo askari jela alitufokea kwa sauti yake yote. "Ingieni si mmeamua kuja huku?" Muda wote huo tulikuwa tusisukumwa kushoto kulia, ili ikiwezekana tufanye kile walichokitaka. Mioyo yetu ilivyozidi kuwa migumu ndivyo mateso na matisho yalivyozidishwa. Pingu zililetwa na tukafungwa pingu wawili wawili. Tulianza safari ya kwenda mahakamani tukilindwa na askari zaidi ya kumi. Nafikiri hata Artur mMargaryani wasingewekewa ulinzi mkali hivyo. Ikaja zamu ya kuzunguka mahakama yote tukielekea kwenye mahakama ya makosa ya usalama trafiki. Tulipoingia tulifunguliwa pingu na kungoja zamu ya kuitwa na kuhukumiwa. Tulionywa kwamba tuwe wasikivu na tutoe sauti kubwa tunapokubali au kukataa kosa. Majina yalipoanza kuitwa, ndipo nilipogundua kwamba wengi waliokuwa wameshitakiwa siku hiyo walikuwa Wakikuyu. Kama ulikuwa umedanganyika ufikiri kwamba Kibaki kuweka Wakikuyu kila kona alikuwa na lengo la kuyanyanyasa makabila yale mengine, basi itakubidi ufikiri upya. Yale niliyoyaona mahakamani ni sawa na Wakikuyu wakikulana wenyewe. Wengi walikuwa wameshitakiwa makosa ya kuendesha magari bila vithibiti mwendo. Wengi walikubali makosa yao huku wakionyesha risiti za vithibiti mwendo, na kudai kwamba magari yao yamewekwa vifaa hivyo lakini askari wameamua makusudi kuwashitaki kwa makosa hayo ya uongo. Jaji alipowauliza kwa nini wanakubali huku wakijua wazi kwamba wameshitakiwa isivyo halali? Majibu karibu yote yalifanana. Walisema ni rahisi kukubali na kulipa faini ya Ksh. 8000 kuliko kusubiri kesi ndefu ambayo hawajui itaisha lini, na mbaya zaidi gharama ya kutetea haki ni kubwa zaidi kuliko faini wanayolipa. Ilipofika zamu yangu, tayari nilijua cha kufanya. Nilikubali kosa, na kwa bahati nikalipishwa faini ya KSHS 2000 tu. Kwangu nilisikia kufarijika kwani ningetoa rushwa ningekuwa nimetoa nyingi kuliko hizo, na kisha roho yangu ingeumia kwani nimetoa rushwa. Kama faraja yangu inamaanisha chochote kwako ni sawa. Kuna wengine wanaosema kwamba zote ni rushwa tu. Serikali inapoamua kutengeneza sheria kwa lengo la kupunguza ajali barabarani na kuongeza ajali hizo kwenye mifuko ya wananchi wake, haiwasaidii wananchi husika. Hatujui ni kwa kiwango gani sheria za Michuki zimepunguza ajali barabarani, lakini kuna jambo moja ambalo halipingiki. Sheria hizo zimewaongezea uwezo askari wa usalama barabarani na sasa wananchi lazima wacheze mikononi mwao. Hata sura zao zinaonyesha kwamba wanaoifaidi biashara ya Matatu ni maaskari wa barabarani kuliko wanaozimiliki matatu zenyewe. Kuna wengine wanasema kwamba siku hizi serikali imehamisha pesa kutoka kwa wenye matatu na kuzihamishia mifukoni wa wana usalama barabarani. Maisha yao yalibadilika ghafla tangu Kibaki aingie madarakani. Kitambo walijulikana kwa kupokea rushwa kuanzia KSHs 20, sasa nasikia hata mia mbili hawachukui. Bei ya RUSHWA imepanda kuanzia shilingi 1000. Wana matatu wanasema siku hizi askari ndiye anayeamua kosa gani akushitaki nalo. Wanajua magari hayakosi makosa. Wakikushika na uongee nao vizuri, wanakuambia utoe sare ya kazi ili ushitakiwe kwa kutovaa sare, nafaini yake ni KSHS1000. Au akikuhurumia sana, atakushitaki kwa kutofunga mkanda, na faini yake ni KSHS 500. Usisahau abiria nao wamo kwenye sakata hilo, jambo linalowaongezea askari mawindo yao. Baada ya hayo yote kufanyika, bado serikali ya Kibaki itawaomba wananchi kura mwaka 2007. Pengine watachaguliwa. Huwezi kujua. Tusubiri tuone.Ni Ukweli kwamba sasa polisi wa usalama barabarani wanakula kuku kwa mrija. Yaani wao ukiwauliza serikali gani iliyowafungulia mifereji ya pesa kumwagika kwao, watakujibu ni serikali ya Narck. Tena watasema Kibaki aitawale Kenya milele. Lakini kwa wananchi wa kawaida sitoshangaa jibu likawa tofauti.
Kinachoumiza roho ni jinsi serikali inavyowanyanyasa wamiliki wa MATATU kiasi cha kutufanya wengine tuamini kwamba kufanya biashara ya MATATU Kenya ni haramu. Kuna wanaosema Serikali Ya Kibaki ni kama suala pekee waliloingia madarakani kufanya ni kuwanyanyasa watu wa MATATU. Kuna Mmasai mmoja aliyenukuliwa akisema kwamba "serikali inatakiwa iagize SPEED GOVERMENT za kuwazuia vijana waache ngono wajiepushe na UKIMWI, kuliko hizo vitu zinaekwaekwa kwenye MATATU." Wabunge kazi yao ni kutunga sheria, siyo kuwaelimisha wananchi sheria hizo. Kosa liko hapo.Wananchi wengi wanaogopa kupoteza muda mahakamani kwa mashauri yasiyoisha. Wananyimwa haki kwa sababu muda wa kuitafuta haki ni mrefu na hawana hakika kama wataipata haki yenyewe. Kwa maoni yangu serikali inapowapa polisi uhuru wa kuitumia sheria kuwanyanyasa wananchi, huo ni wizi wa mchana. Tofauti yake na wizi wa mabavu ni kwamba serikali inatumia sheria ambazo wananchi hawazijui ili kuwaibia. Na kwa kiwango hiki, serikali ndiye mwizi nambari wani.Majaji wanatakiwa kupima uzito wa shauri hata kama mshitakiwa amekubali kosa. Mazingira yanayomfanya akubali kosa yaangaliwe na ikiwezekana ushahidi kidogo utolewe na polisi husika ili washukiwa waachiliwe huru hata baada ya kukubali makosa. Mambo yakiwa hivyo tunaweza kusema Haki inaonekana kutendeka japo kidogo.Sheria zikiwepo ili kuwanyima wanyonge haki, basi wanajaribu kuzitii sheria wanakosea kufanya hivyo. Huwezi kutii kitu ambacho kuna watu wanaoweza kusema umekivunja na wakunyime haki ukiona na usiwe na pa kuwapeleka wala cha kuwafanya.Inauma kuliko ukoloni. Tena ni mbaya kuliko ubaguzi wa rangi.Ubaya wake unazidi pale wanaofanyiwa unyama huo ni wananchi wanaodanganywa kwamba wanaishi katika Kenya huru. Uhuru huo uko wapi wakati haki haitendeki? Tangaza na GTV
|
||||||||||||
|
|
|
|